Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) –ABNA– Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, katika ujumbe wake wa rambirambi kufuatia kifo cha Ayatullah Al-Udhma Wahid Khorasani, amemtaja marehemu kuwa miongoni mwa nguzo kuu za ufundishaji wa Fiqhi na Usuli Fiqhi katika Hawza za Elimu ya Dini.
Ifuatayo ni sehemu kamili ya ujumbe huo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
Nimepokea habari za kuaga dunia kwa mwanazuoni na mwalimu mkubwa wa Hawza za Elimu ya Dini, Ayatullah Al-Udhma Wahid Khorasani. Hakika mwanazuoni huyo mkubwa alikuwa miongoni mwa nguzo kuu za ufundishaji wa Fiqhi na Usuli Fiqhi katika Hawza za Elimu ya Dini.
Katika miongo ya hivi karibuni, vipindi vyake viwili vya kila siku vya kufundisha vilikuwa miongoni mwa vikao muhimu na mashuhuri zaidi vya masomo katika Hawza. Katika vipindi hivyo, pamoja na uchambuzi na tafiti zake binafsi za kitaaluma, alidhihirisha kwa uwazi umakini mkubwa, uelewa wa kina na kuthamini maoni ya baadhi ya wanazuoni mashuhuri wa zama za hivi karibuni katika Hawza ya Najaf Ashraf, sambamba na umahiri wake mkubwa katika kuyafahamu maoni hayo.
Sifa hii, ikiambatana na namna yake nzuri, yenye mpangilio na hoja madhubuti katika kufundisha, ilifanya kila kipindi cha darasa lake kuwa fursa yenye manufaa na yenye thamani kubwa kwa wanafunzi na watafutaji wa elimu.
Kwa sasa, idadi kubwa ya walimu na wanazuoni katika Hawza ya Qum, na hata katika Hawza nyingine nchini, pamoja na kundi la wanazuoni wa miji mbalimbali, wanajivunia kuwa waliwahi kuhudhuria vipindi vya masomo ya mwanazuoni huyo katika historia yao ya kielimu.
Aidha, wote wanamtaja kwa heshima na pongezi kutokana na jinsi alivyoonesha kwa dhati na kwa uwazi katika maneno na mwenendo wake, kipengele cha kujifunga na kujisalimisha kwa dhati kwa Maimamu Watoharifu (a.s.).
Bila shaka, kutokana na juhudi zake za muda mrefu na endelevu katika kuitumikia Sharia na madhehebu, mwanazuoni huyo ana haki kubwa juu ya jamii ya waumini na Hawza za Elimu ya Dini, ambayo kila mmoja anapaswa kuitambua na kuithamini.
Mimi binafsi, ninatoa pole kwa msiba huu kwa Bwana wetu Imam Mahdi (a.j.), Hawza za Elimu ya Dini, waumini wote, na hususan familia tukufu ya marehemu. Namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amjaalie marehemu daraja za juu kabisa.
Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei
(17 Novemba 2026)
Maoni yako